MWINGILIANO WA MAFUMBO NA MAUDHUI YA UONGOZI KATIKA NYIMBO ZA SITI BINTI SAAD

Makala hii ilichunguza Taarab hususani tungo za Siti Binti Saad. Kipengele cha Mtindo ambacho kiliangaliwa katika utafiti huu ni mafumbo. Vilevile, tumeangalia jinsi mafumbo yanavyoendeleza maudhui na dhamira katika utunzi wa nyimbo za Siti Binti Saad. Aidha, tumefumbua mafumbo mbalimbali katika nyimbo hizi. Suala la mafumbo na mandhari pia limejadiliwa kwa kina. Je, mandhari yana athari yoyote katika mafumbo ya Siti Binti Saad? Swali hili limeibua swali jingine – je, mafumbo ni jambo la mwandishi au jamii? Haya maswali yemejibiwa katika mawasilisho ya uchanganuzi wa data. Huu ni utafiti wa mtindo katika nyimbo za Taarab na umefanywa kwa kuzingatia mihimili ya nadharia ya Mtindo na ya Semiotiki. Nadharia ya Mtindo iliasisiwa na Buffon katika mwaka wa 1930 na kuendelezwa na Coombes na Leech katika mwaka wa 1969. Mtindo unahusu jinsi mtunzi anavyojieleza kwa kutumia lugha. Mtindo ni muhimu sana katika kazi yoyote ya fasihi kwa kutokana na mchango wake katika kuwasilisha ujumbe. Utafiti ulifanywa maktabani, nyanjani na kwenye wavuti. Data iliteuliwa kwa njia ya nasibu na kimakusudi kwa sababu ililenga mutribu mmoja ambaye nyimbo zake zinajulikana tayari. Aidha, tulitumia mahojiano, vitabu, makala mbalimbali na tasnifu za watafiti wengine ili kutoa maelezo zaidi kuhusu data. Ilijitokeza kuwa mafumbo husaidia katika kuwasilisha mawazo au hisia za mtu kwa njia ya upole bila kuleta mhemko au mabishano baina ya watu. Ni njia moja ya kusema bila makali ya maneno. Isitoshe, ilidhihirika kuwa mafumbo ni njia mojawapo ya mitindo yauimbaji wa Taarab ya asili.

Maneno muhimu: Ufakiri, mafumbo, usawiri, dhuluma na utabaka